| italiano | english | swahili | português |
   
 

 

SINTESI STORICA E CRONOLOGIA ESSENZIALE
CANTI
BIBLIOGRAFIA
LA CAUSA DI BEATIFICAZIONE
DOVE SIAMO

home | mail | guestbook | links

Mtunzi: Renato Riccioni (Mtetezi wa Utakatifu wao) - Mfasiri: nd. Rikardo Maria Riccioni

1. KUZALIWA KATIKA MPANGO WA MUNGU

Antonia Faioli alipozaliwa, Dada Watatu walikuwa pamoja kwa mara ya kwanza. Siku hiyohiyo, tarehe 10 Juni 1723, katika kanisa la Mt. Petro, Teresa (8) na Sesilia (4) walihudhuria Ubatizo ambao mdogo wao alipewa na paroko Alexanda Alessandri. Ingawa kulikuwa na furaha ya kidini kwa kumpokea mtu mwingine katika familia kubwa ya Mungu, kuna uwezekano mkubwa kwamba wakati huo hata mmoja alitambua huo ulikuwa mwanzo usiotabiriwa wa maisha ya kidugu, ya kuwa pamoja daima kwa hao watatu, ambao ni fundisho halisi la maisha ya kijumuia. Tangu siku hiyo ya karne zilizopita hayo yanaendelea kuzaa mema mengi.

 

2. KUTEMBEA KIFAMILIA

Kila Jumapili – siku ya Bwana – Misa ilihudhuriwa na familia nzima ya Faioli.
Hivyo imani ya watoto ilistawi ikisaidiwa na mifano ya wazazi waliotekeleza mafundisho yao.
Kwa hakika furaha ya mabinti hao watatu ilikuwa kubwa katika mpando wa muda mfupi toka nyumbani kwao hadi kanisa la parokia ya Mt. Stefano, walipongojewa na abati Rosa, mjomba wao, lakina hasa na Yesu. Ni kama tunawaona, hao watatu, wakikua pamoja! Teresa na Sesilia, wakipanda ngazi pana, kwa aina ya liturujia ya kifamilia, walikuwa wanamshika mkono Antonia, mdogo wao, wakirudiarudia ishara ya msalaba na mashauri mengine ya kufaa.

 

3. KUJIFUNZA ILI KUSTAWI

1715-1727. Ingawa habari kuhusu sehemu ya kwanza ya maisha ya Dada Watatu ni chache, si vigumu kujichorea muda waliojifunza kuishi nyumbani mwao: ibada zao za kwanza, maelekezo ya msingi kuhusu maisha ya pamoja, mang'amuzi mbalimbali ya ushirikiano katika kazi za kila siku. Hasa Teresa aliweza kufaidika na miaka 12 ya thamani aliyoishi karibu na mama, akawashirikisha Sesilia na Antonia matunda yake. Mama Marta mwenyewe, aliyekuwa na shamba ilipolimwa pia aina ya pamba, huenda akawaachia wanae watakaokuwa Watawa Walimu kitanda cha mfumi ambacho wakajitolea kwa ukarimu kitumiwe na wanafunzi wao.

 

4. KUTESEKA PAMOJA

Ilionekana ni miadi ya uhai: kila baada ya miaka minne familia Faioli ilikuwa inamngojea kiumbe mpya aliyeitwa kuingia fumbo la maisha: hivyo, mwaka mzima wa 1727 ulitawaliwa na tarajio la namna hiyo.
Mang’amuzi hayo yalikuwa mapya kwa Antonia, marudio kwa Sesilia, yenye uelewa zaidi kwa Teresa, aliyejiandaa kumsaidia mama vizuri zaidi na zaidi katika majukumu yanayoongezeka.
Yalijirudiarudia maswali ya kawaida lakini mapya daima: wa kiume au wa kike?
Maandalizi yalizidi kufanyika, likachaguliwa jina zuri zaidi… Maria.
…Lakini, wakati wa kujifungua, kuna shida fulani: mtoto anashindwa kuishi. Hata mama ana matatizo…

 

5. KUAMINI ZAIDI…

Sikitiko kubwa kwa mdogo wao Maria kufa muda mfupi baada ya kuzaliwa lilifuatwa mara na lingine la kuvuruga akili zaidi: siku ileile ya mazishi ya mtoto, mama yao Marta alifariki pia! Ilikuwa tarehe 22 Oktoba 1727. Wakiwa wameduwaa, Teresa, Sesilia na Antonia, walihudhuria pamoja na ukoo mazishi ya mama yao katika kanisa la Mt. Blasi. Lakini mang'amuzi hayo, yasiyoeleweka kwa yeyote nje ya Ufunuo wa Mungu, yakachangia kuwafanya wakomae kabla ya wakati na kushikamana kwa uimara. Yesu tu, ambaye alikufa akafufuka, aliweza kuwarudishia hao mabinti watatu wasiofarijika tumaini na nguvu ya kukabili maisha.

 

6. KUJIIMARISHA ILI KUTOA USHUHUDA

Kwa kifo cha mama Marta, maisha ya Teresa, Sesilia na Antonia kwa hakika yalipata kuwa magumu zaidi, lakini hayakukoma.
Wala tukio hilo la kusikitisha halikudhoofisha imani ya familia Faioli: miezi michache baadaye, tarehe 15 Juni 1728, Sesilia na Antonia pia wakapokea Kipaimara kwa mwakilishi wa askofu. Sakramenti hiyo, kwa kuwamiminia zaidi vipaji vya Roho Mtakatifu, ikawawezesha kukabili mapambano mapya ya maisha, na kushuhudia imani ya Kikristo katika ulimwengu ambao watakuja kuufahamu katika miaka ya ubalehe; wakiunganishwa na Roho, wataukabili kwa busara na ari.

 

7.KUWASIKILIZA WANAOPENDEKEZA WEMA

Katika wiki za uamsho, zilizofanyika kila baada ya miaka michache, wahubiri bora walijitahidi kuchochea na kuunda dhamiri za waamini, wakihimiza uongofu wao pamoja na kutokeza maitikio motomoto kwa wito wa kitawa. Akina dada Faioli, wakishiriki wiki hizo zilipofanyika Anticoli mnamo Juni 1741, wote watatu walikuwa tayari kusikiliza maneno ya wahubiri shujaa Struzzieri na Giannini, hata wakaamua kumtolea Mungu maisha yao yote. Itikio lao kwa wito likawa pia la msingi kwa uanzishwaji wa Shirika jipya la kitawa na kwa utume wake karne zijazo.

 

8. KUTAMBUA MAONGOZI YA MUNGU

Hao Dada Watatu, wakipania kustawisha maisha ya sala katika nyumba ya njia Vetere, walipokuwa wanaishi pamoja na Arkanjelo, hawakuweza kuhisi kazi ambayo Mungu alikuwa akiwaandaa kuifanya, lakini kwa hakika Maongozi yake yaliwasaidia kwa kuwatolea mazingira ambapo wataianza. Mnamo Novemba mwaka uleule, Abati Rosa,
akihisi mwisho wa maisha yake unakaribia, aliamua kuandika wasia na kuacha mali yake yote kwa mpwa wake Teresa, ambaye labda alimsaidia katika ugonjwa wa mwisho.
Tendo hilo la padri linaonyesha alivyothamini na kutegemeza chaguo la maisha ya kitawa la wote watatu. Halafu akafa.

 

9. KUWAPOKEA WANAOLENGA WEMA

1741-1747. Inawezekana sana kwamba Teresa, Sesilia na Antonia walipotawa nyumbani mwao ili kujitoa kwa Mungu tu, hawakuwaza wasichana wengine watavutiwa na mfano wao. Kumbe wengi waliwatafuta na kuwateua wawafundishe namna ya kuishi, kwa sababu walitaka kujifunza toka kwao. Kwa miaka sita shule hiyo ya pekee iliyojiotea ilizaa matunda ya mti mwema.
Kutokana na karama ya malezi ya Akina Dada Faioli, sala, katekesi, ufundishaji wa kusoma na kufanya kazi za kike vilistawisha heshima ya wanawake na ya familia.

 

10. KUTOOGOPA MATATIZO

“Aina ya shule” ya Akina Dada Faioli ilianza,na matatizo yakaanza, kama ilivyo kwa kazi zote wa Mungu.
Paroko mpya, aliyeteuliwa badala ya mjomba wao, ndiye aliyefungua kesi dhidi ya Teresa, akimdai majengo jirani na parokia. Hivyo, mwaka 1742, msichana huyo, akiongozana na kaka yake, alijikuta mahakamani ameshtakiwa. Kesi ikachukua miaka.
Kwa hakika paroko alikuwa na shida - pia kwa sababu ya ufukara mkubwa wa wengi kule nyakati zile - lakini tuzingatie hasa hao watatu walivyokuwa na nguvu ya kustahimili, wasijali mazingira ya upinzani: kosa lao lilikuwa tu kupokea urithi walioutumia kutendea mema.

 

11. KUTHIBITISHA KARAMA

Wote walijua fika kwamba ngao ya Askofu iliyowekwa katika mlango wa nyumba ya Akina Dada Faioli, haikuwa pambo tu. Jumatatu ya tarehe 16 Oktoba 1747, Askofu Bacchettoni, akiwa na wasaidizi wawili, aliingia ile nyumba-shule ili kuwachunguza mmojammoja hao walimu vijana, kanuni zao, sala zao n.k. Akatoka ameridhika akiwa tayari kuitegemeza shule hiyo kwa maamuzi mapya na kwa kuitetea hata mbele ya Papa Benedikto XIV. Hivyo Kanisa lilipima na kuthibitisha kazi iliyoanzishwa na Dada Watatu likikubali rasmi karama ya kila mmojawao.

 

12. KUSONGA MBELE KWA BIDII

Kwa maongozi ya Mungu, padri mkuu Girolami, aliyeteuliwa na askofu kufuatilia ustawi wa kazi iliyoanzishwa na Akina Dada Faioli, alipoingilia kati alifaulu kuweka kando mivutano iliyokuwepo. Ujio wa Dominika Tardioli, aliyejitolea jengo aliloachiwa, pamoja na kubadilisha vyumba vya shule ya awali, ulileta mahali pakubwa zaidi, tena katika parokia ya padri Dominiko, mtetezi wao. Si vigumu kujichorea hali ya maandalizi, pamoja na uhamisho wa mali yote ya Dada Watatu walioona hivyo uwezekano wa kupata hali mpya, ya kufaa zaidi kwa maisha na utume wao.

 

13. KUKUMBATIA UTUME

Jioni ya Noeli mwaka 1747 maandamano yasiyo ya kawaida yalipitia njia kuu ya Anticoli yakiongozana na akina dada Faioli pamoja na msichana Domenika Tardioli na mtoto Roza Girolami hadi makao mapya ya shule ya Bweni. Siku hiyo takatifu, iliyong'ariza tumaini kwa wote, mahali fukara kama pango la Bethlehemu lakini palipo tayari kwa kazi iliyopangwa na Mungu, palipokea mwanzo wa Taasisi hiyo iliyokwishajaribiwa muda mrefu. Padri Dominiko Girolami, aliyefurahi kuteuliwa Mkurugenzi wake, alibariki majengo yale ambayo yakaja kupanuliwa na kubaki Nyumba Mama ya Shirika jipya.

 

14. KUMTEGEMEA MUNGU

Siku chache baada ya kutamalaki nyumba mpya, tazama, Teresa na msichana Dominika walipaswa kuondoka. Nyumbani, katika matatizo ya uhamiaji, walibaki tu Sesilia na Antonia, pamoja na mtoto Roza. Tufikirie ugumu wa kutengana: ni mara ya kwanza (na ya mwisho) ya Akina Dada hao kujua itawabidi kukaa mbalimbali kwa muda mrefu.
Sadaka hiyo haikukosa uchungu, tukizingatia Teresa alikuwa nani kwa wadogo wake wawili, na Sesilia na Antonia walikuwa nani toka mwanzo moyoni mwa Teresa, pamoja na matatizo na mambo yasiyotarajiwa ambayo yakabiliwe kwa imani.
Utengano huo utazidi kuwaunganisha Dada Watatu na Mungu.

 

15. KUFUATILIA MALEZI

Maisha ya kitawa, na hasa uanzishaji wa Shirika, vinadai misingi imara. Tarehe 7 Januari 1748, Teresa Faioli na Dominika Tardioli waliondoka Anticoli waende Anagni kwenye Ikulu maarufu ya Mapapa. Kwa miezi mitano walipokewa huko kwa ukarimu na Masista Wasitoo wa Upendo, ambao tangu miaka mingi walikuwa wakilea wasichana wa Anagni. Kwa hao wawili ikawa aina ya unovisi na mang'amuzi azizi ambayo waishirikishe Jumuia yao. Kwa wenzao, waliobaki muda mrefu peke yao bila ya mawasiliano rahisi, wakati huo ukawa jaribio la kufaa la ukomavu wao.

 

16. KUJINYIMA YOTE ILI KUPATA YOTE

8 Novemba 1749. Kwa hati rasmi iliyoandikwa mbele ya wakili, Dada Watatu na wenzao wawili walitoa mali yao yote kwa Shirika jipya. Kujinyima hivyo kila kitu sio tu tendo la ukarimu bali pia thibitisho wazi la imani lenye kustahili, hasa kutokana na hali ya mashaka ya Taasisi na ufukara wa mahali ilipoanzia. Upendo na imani tu vinawezesha kujinyima vyote. Majitoleo ya hao wanawake wakarimu wa kwanza yakawezesha kuunda rasmi Bweni hilo litakalotazamiwa na walei na wachungaji wa majimbo mengine kwa tumaini. Cheche hiyo nyenyekevu na nyamavu itapamba moto.

 

17. KUendelea kati ya matatizo

Askofu Monti, alimuandikia barua Contestabile Colonna, akisimulia alivyokutana na wasichana wa Bweni, mnamo Agosti 1752, na alivyoona hali ngumu, ufukara, afya mbovu na wasiwasi. Kwa kweli, Jumuia ilikuwa imejaribiwa na haja ya padri Girolami kukaa mbali, huko Roma, kwa ajili ya kesi itakayothibitisha hana makosa aliyoshtakiwa na Ofisi za Jimbo la Anagni.
Hata hivyo muda huo mrefu wa kumkosa huyo aliyekuwa sio tu mratibu na mtetezi, bali pia mwadhimishaji na kiongozi wa Kiroho,
ulipitwa na Dada Watatu kama jaribio halisi la uwezo wao wa kudumu kwa vyovyote, wakiendelea kulifanyia kazi Kanisa, wasikate tamaa.

 

18. KUKUBALI MAJARIBU

Uchungu wa msalaba uliendana na ustawi wa Taasisi ya Anticoli pia. Padri Girolami alilalamikia matatizo, dhana potovu na dhuluma dhidi yake na ya Bweni... kama vile utovu wa wema aliouonyesha Askofu Monti alipofanya ziara ya kichungaji tarehe 2 Julai 1753 ambayo ilifikia kilele alipokuta nguruwe mdogo akifugwa katika handaki chini ya nyumba ya kitawa. Pamoja na vipengele vingine vilivyochorwa na kumbukumbu za ziara, huo ulikuwa ushahidi wa maisha fukara sana na ya sadaka. Lakini hakuna kilichoweza kulegeza juhudi za hakika na udumifu wa hao Waanzilishi motomoto. Miaka michache baadaye, hata mhashamu Monti alisahihisha mitazamo yake.

 

19. KUVUMILIA KATIKA MAPAMBANO

Asiyejua masharti ya maisha ya kitawa anaweza akashangaa juhudi kubwa za Jumuia kwa ajili ya kulinda hali ya kujitenga na kujikusanya.
Kwa kweli Nyumba yao, iliyokuwa kwenye njia kuu ya Anticoli, haikuweza kuepa masumbuko ya aina mbalimbali… yakiwa ni pamoja na kelele zenye kufuru za klabu ya karibu na matendo yasiyo na ustaarabu ya majirani.
Lakini dhihaka, matusi, vituko vya ulimwengu na upinzani wowote uliotaka kuvuruga amani ya maisha yao, viliruhusiwa na Mungu ili kuwatenga na maisha ya dunia hii na kuwafanya watamani zaidi na zaidi siku ya kukutana naye milele.

 

20. KUSHINDA KWA USTAHIMILIVU

Miaka kumi iliyofuata ziara ya kichungaji ya mwaka 1753 ilidhihirisha kuwa muda unahitajika ili kukata shauri vizuri.
Tarehe 7 Februari 1763 ujumbe kwa Wanabweni uliarifu kwamba Askofu Monti ameamua kwa wema kuwalipia shela za Watawa Walimu. Ni rahisi kutafsiri tendo lake kuwa utambuzi usio rasmi wa uwezo wao wa kutimiza kazi hiyo ambao hapo awali mwenyewe alikuwa ameutilia shaka. Tujichoree wote walivyoridhika kwa dhati kuvaa shela hizo baada ya miaka mingi ya kudhalilishwa waziwazi

 

21. KUPOKEA MIZIGO

Si vigumu kujichorea wasiwasi ulioipata Jumuia Mama mkuu Angelika Bertoni alipojiuzulu mbele ya Askofu mpya, Sirili Antonini, aliyeonekana kulitazama Bweni kwa wema mkubwa.
Ni ya maana zaidi kuzingatia kwamba katika nafasi hiyo ngumu, iliyohitaji chaguo la hakika, masista walimchagua kwa kauli moja Antonia, mmojawapo kati ya Waanzilishi.
Ilikuwa tarehe 6 Machi 1779. Katika orodha ya waliohudhuria mkutano huo linakosekana jina la Teresa: labda alikuwa mgonjwa. Hivyo Sesilia na Antonia walijiandaa kukabili bila ya dada yao hatua muhimu ya kuunda moja kwa moja Shirika.

 

22. KUELEKEA MBINGUNI

Teresa alipofariki tarehe 14 Julai 1779, baada ya ugonjwa ulioandaa utengano, maisha ya pamoja ya Akina Dada Faioli yalionekana kwisha. Kumbe yakaendelea hata baada ya kuvukia uzima wa milele kwa dada aliyekuwa daima dira ya hakika kwa Sesilia na Antonia. Katika nafasi ngumu zaidi ya maisha ya Taasisi, Antonia alichaguliwa na Jumuia ashike usukani, huku Sesilia haachi kutoa mashauri yake yenye busara. Ustawi uliofuata wa Familia ya kitawa ukathibitisha mafanikio ya wito wa pamoja ulioitikiwa na Dada Watatu kwa mshikamano wa kiroho wa pekee.

 

23. KUWA WAPYA KADIRI YA ROHO MTAKATIFU

Baada ya kupata mashauri ya watu wa Mungu, Askofu Sirili Antonini aliwapokea Watawa Walimu kumi wa Bweni la Anticoli waanze kuvaa kanzu ya Mt. Klara na kuweka nadhiri ya useja mtakatifu. Ibada hiyo ya fahari ilifanyika katika kanisa la Mt. Petro tarehe 23 Agosti 1781. Hivyo kwa Sesilia na Antonia ikawa rasmi hali walioiishi tangu ujanani, sawa na Teresa, wakijitoa kabisa kwa Mungu, bila ya kujibakizia wala kuangalia nyuma. Askofu mwenyewe akatunga kanuni mpya kwa kulinganisha ile ya Mt. Klara na madai ya karama ya malezi iliyo maalumu kwa Taasisi mpya.

 

24. KUELEKEZA KWENYE UBORA

Ilipita miaka michache tangu uvaaji wa kanzu ageuze hali ya Walimu wa Anticoli kutoka ile ya kuwa aina ya walei waliojitoa mhanga hadi ile ya kuwa watawa halisi. Ili adumishe Shirika lao moja kwa moja, Askofu Sirili Antonini alipendekeza kanuni yake badala ya ile iliyoandikwa na padri Girolami.
Tarehe 27 Juni 1785 ulifanyika Mkutano wa Jumuia ili kukubali au kukataa huo mpango mpya.
Hata katika nafasi hiyo muhimu sana kwa mwelekeo wa Shirika, Antonia alileta uzito wote wa mamlaka ya kiroho ya Waanzilishi, na waliohudhuria, mmojawapo akiwa Sesilia, wakakubali kwa kauli moja.
Ndivyo walivyozaliwa Masista wa Imakulata wa Mt. Klara.

 

© 2007 - Congregazione delle Suore dell'Immacolata di Santa Chiara
- DIADAIN consupertrafra -